"WATENDAJI WA VIJIJI FANYENI SENSA KUJUA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM ILI WAENDE SHULE-WAZIRI MKUU
NEWALA.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wa watoto wenye
mahitaji maalumu kutowafungia ndani na badala yake wawapeleke shule.
Amesema ulemavu si kigezo cha kuwakosesha watoto hao kupata elimu na kufanya kazi, hivyo amewataka jamii kutowakatisha tamaa
Alitoa
agizo hilo wakati alipokagua mradi wa
ujenzi wa majengo ya chuo cha Ualimu Kitangali, kilichopo Newala mkoani
Mtwara.
“Watakaobainika
kuwafungia ndani watoto wenye mahitaji maalumu wachukuliwe hatua za
kisheria kwa sababu wanawakosesha haki ya kupata elimu.”
Pia
amewaagiza watendaji wa vijiji wafanye sensa katika maeneo yao ili
kubaini idadi ya watoto hao na watakapofikia umri wa kwenda shule
wapelekwe.
Waziri
Mkuu alisema Serikali inataka watoto wenye mahitaji maalumu watambulike
pamoja na mahitaji yao na waliofikia umri wa kwenda shule wapelekwe.
“Tunataka
kila mtoto wa Kitanzania aliyefikia umri wa kwenda shule apelekwe shule
na kusoma na wenzake. Serikali imeboresha elimu ili watoto wote
wasome”.
Alisema
watoto wenye mahitaji maalumu wana haki sawa na wengine, hivyo hakuna
sababu ya kuwafungia ndani na kuwakosesha kupata elimu.
Kwa upande wake, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo
alisema mradi huo unahusisha ujenzi na ukarabati wa vyuo vinne vya
ualimu.
Dkt.
Akwilapo alivitaja vyuo hivyo ni Ndala cha Tabora, Mpuguso cha Mbeya,
Kitangali cha Newala na Shinyanga, ambapo ujenzi utagharimu sh. bilioni
36.47.
Alisema
mradi huo wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo hivyo vinne
utaleta tija kubwa kwa Serikali katika kuongeza fursa za kutoa mafunzo
ya ualimu katika ngazi za stashahada na shahada.
“Vyuo
vyote hivi vinne vitakapokamilika vitakuwa na uwezo wa kudahili
wanachuo 3,300 kwa wakati mmoja kutoka uwezo wa sasa wa kudahili
wanachuo 1,855”.
Akizungumzia
kuhusu chuo cha Kitangali ambacho kilijengwa 1937, alisema kinajengwa
upya kutokana na uchakavu wake kiasi cha kutofaa kufanyiwa ukarabati.
Awali,
Kaimu Mkuu wa chuo hicho Mwalimu Emmanuel Haule alisema Serikali kwa
kushirikiana na Canada zimetoa sh. bilioni 8.26 za ujenzi wa
miundombinu.
Mwalimu
Haule alisema miundombinu inayojengwa chuoni hapo ni pamoja na vyumba
vya madarasa, mabweni, nyumba za watumishi na maabara.
“Pia
tunajenga ukumbi wa mikutano na ukumbi wa mihadhara, maktaba na
uchimbaji wa kisima cha maji. Ujenzi unatarajiwa kukamilika Aprili 26,
2018.
Source.pmo/triplea fm habari-28.02.2018
Post a Comment