VIONGOZI TANDAHIMBA DHIBITINI MIMBA KWA WATOTO WA SHULE-PM MAJALIWA
TANDAHIMBA.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Tandahimba kuhakikisha
inadhibiti ongezeko la mimba kwa watoto wa shule.
Ameyasema hayo leo (Jumatano,
Februari 28, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri
ya wilaya ya Tandahimba.
Waziri Mkuu amesema ni lazima
viongozi hao wasimamie nidhamu kwa kuwalinda watoto wa kike katika wilaya hiyo
wasipate mimba ili waendelee na masomo.
“Kwa nini kila mwaka mimba Tandahimba
zinaongezeka, viongozi simamieni utekelezaji wa sheria kwa kuwachukua hatua
wote waliowapa mimba wanafunzi.”
Amesema lazima wahusika wote
wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kwa sababu wanaharibu elimu
ya motto wa kike jambo ambalo si zuri.
Waziri Mkuu ametolea mfano
mwaka 2015 wafunzi 10 walipata mimba, mwaka 2016 waliopata mimba walikuwa 20,
mwaka 2018 waliongeza na kufikia 57.
Amesema takwimu hizo
haziridhishi, hatua kali zichukuliwe kudhibiti vitendo hivyo na Serikali
haitaki kusikia mwanafunzi ameacha shule kwa sababu ya kupata mimba.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi
wa umma wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na wafuate sheria.
Waziri Mkuu ambaye yuko
mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi amewasisitiza watumishi wa umma wawafuate
wananchi vijijini na wawahudumie
ipasavyo.
Amesema Rais Dkt. John Magufuli
amesisitiza watumishi wa umma wawatumikie wananchi bila ya ubaguzi wowote
pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
“Serikali inataka kila
mtumishi atimize wajibu wake na haina muda wa kuwalea watumishi wazembe, wala rushwa
na wasiowajibika, hivyo watambue wajibu wao.”
Source.pmo/tripleafm habari-28.02.2018

Post a Comment