WABISHI SASA KUJENGA VYOO CHINI YA USIMAMIZI WA POLISI SUMBAWANGA
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amesema atalazimika
kuwatumia polisi kusimamia zoezi la usafi na ujenzi wa vyoo salama katika Kijiji
cha Namasinzi, kata ya Kapenta, bonde la ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga baada
ya wananchi hao kushindwa kujenga vyoo hivyo mbali na elimu ya umuhimu wa vyoo waliyopewa
kwa muda mrefu.
Amesema kuwa ikifikia hatua hiyo Kijiji hicho kitafungiwa na
hakuna atakayetoka wala kuingia na hatimae kusitisha shughuli za kiuchumi za Kijiji
hicho ambacho ni maarufu kwa kilimo cha mpunga hali itakayopelekea maisha
magumu kwa wananchi hao jambo ambalo asingependa litokee.
Katika kuhakikisha hali hiyo haitokei Mh. Wangabo alimuagiza
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule na timu yake ya usafi ya
halmashauri kuhakikisha wanapita kaya kwa kaya ili kuzibaini kaya zisizopenda
usafi na zisizokuwa na vyoo na kuzichukulia hatua za kisheria kwani kwa
kushindwa kufanya hivyo kipindupindu hakitamalizika katika bonde hilo.
“Sasa tutatumia nguvu ya dola, ili kuhakikisha kwamba kila
mtu anaishi katika maisha ya usafi wala sio uchafu, na kila mtu ahakikishe kwamba
anakuwa na kiboko Fulani ambacho ni kigumu amuone mtu anachemsha maji,
anayaweka maji yake yanapoa akienda shambani anakwenda na maji mbayo yamekwisha
poa, lakini mkilea lea hivi, waswahili wanasema ukicheka na nyani unavuna
mabua, mabua ambayo tunayavuna ni vifo.” Alisisitiza.
Aliyasema
hayo katika Mkutano wa hadhara alioufanya katika kijiji cha Namasinzi,
Kata ya Kapenta, Wilayani Sumbawanga, kijiji ambacho wananchi watatu
wamefariki kwa ugonjwa wa kipindupindu na wengine wakiendelea kupatiwa
huduma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hlamshauri ya Wilaya ya
Sumbawanga Dkt. Fani Musa aliendelea kuishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka
misaada katika bonde hilo ili kuhakikisha wanakabiliana na ugonjwa huo na
kusisitiza kuwa wataendelea kutoa elimu bila ya kuchoka akiamini kuwa wananchi
hao wataelewa wakiendelea kusimamiwa.
“Serikali imekuwa ikifanya kazi tatu kwa wakati mmoja,
tumekuwa tukitoa elimu ya ugonjwa huu kwa lengo la kuzuia haya yasitokee,
lakini yakitokea tunatumia nguvu kubwa ya kukabiliana na tatizo hili lakini pia
serikali inatoa dawa za kutosha ili kuweza kuponya pia, ugonjwa wa kipindupindu
ni kitendo cha kula kinyesi ambacho ni kibichi, hivyo watu ni muhimu kujenga
vyoo salama,” Alimalizia.
Tangu kulipuka kwa ugonjwa huo tarehe 6 Mei, 2018 watu 14
wameshafariki na wengine 221 wakiendelea na kupatiwa matibabu katika kambi za
wagonjwa hao katika bonde la ziwa Rukwa, Wilayani Sumbawanga.


Post a Comment