WANAFUNZI 252 SEKONDARI NA 81 MSINGI WAPATA UJAUZITO 2016/17 ARUSHA




ARUSHA.
Ongezeko  la mimba mashuleni limeonekana kukua kwa kasi katika Mkoa wa Arusha baada ya wanafunzi 333 kupata ujauzito kwa mwaka 2016/2017,  wanafunzi 252 wakiwa wa sekondari na 81 shule za msingi.

Hayo yamesemwa na Afisa elimu Mkoa wa Arusha Gift Kyando wakati  akitoa taarifa ya elimu Mkoa kwa kamati ya ushauri ya Mkoa amesema kuwa licha kutoa  taarifa Polisi bado idadi kubwa ya watuhumiwa hawajachukuliwa hatua zozote za kisheria hivyo hatua za makusudi zinahitajika katika kutatua jambo hilo.

Kaimu Mwenyekiti wa katimati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Monduli Iddy Kimanta amesema kuwa katika maeneo ya kifugaji kumekuwa na tabia ya watoto wa Kike kusema wamebakwa lakini baada ya miezi miwili wanakuwa wameolewa hivyo ni vyema kamati hiyo ikafuatilia na kuamua nini kifanyike ili kutatua changamoto hiyo inayokwamisha upatikanaji wa elimu kwa watanzania.

Mkuu wa wilaya ya Arusha Fabian Daqarro amesema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo baada ya kuona kuna tatizo la wanafunzi kupewa ujauzito wameiagiza halmashauri kuwapima wanafunzi kila baada ya miezi mitatu ili kuzuia tatizo hilo kutokana na sheria zinazowalinda watoto na wanafunzi kuvunjwa  na baadhi ya watu.

Ameeleza serikali ya awamu ya tano inagharamikia elimu kwa zaidi ya billioni   23 kila mwezi kwaajili ya kusaidia wanafunzi wote kusoma  na juhudi hizo za serikali zitakuwa  hazina maana kama wanafunzi wataendelea kupewa ujauzito na kudanganywa hivyo hivyo wazazi na walezi wahakikishe wanaiunga mkono serika kwa kuwawekea wanafunzi mazingira wezeshi na kuwapa nafasi ya kusoma.

SOURCE.TRIPLE A FM HABARI-MACHI 8 2018

No comments

Powered by Blogger.