WAATHIRIKA WA MAFURIKO WA MARA KWA MARA JIJINI ARUSHA WATOA KILIO KINGINE






 ARUSHA.

Wakati mvua za masika zikianza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini;Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Kambi ya Fisi Kata ya Ngarenaro jijini Arusha wanahofia usalama wa maisha yao kufuatia mfereji mkubwa wa mkondo wa maji ulioelekezwa katika makazi yao.

Wakizungumza na Radio Triple A wakazi hao wamesema kilio chao ni cha muda mrefu na pia ni changamoto kubwa kwao; hivyo wameiomba serikali kupitia mamlaka husika kulipatia ufumbuazi suala hilo kwa haraka kabla hawajafikiwa na adha ambazo zimekuwa zikiwakumba kila kinapowadia kipindi cha mvua.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kambi ya Fisi Bwana Hillary Mkony amesema viongozi wakishirikiana na wakazi wa mtaa huo wamekuwa wakijitolea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kujenga vivuko lakini kutokana na wingi wa maji nyakati za mvua bado ni changamoto kubwa kwao.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Ngarenaro Isaya Doita amemuomba Meneja wa TANROADS kwa kushirikiana na wataalamu wake kuharakisha ujenzi wa mtaro huo kabla ya mvua za masika ili kunusuru maisha ya wananchi hao.

Meneja wa TANROADS Arusha Mhandisi John Kalupale amekiri kupokea malalamiko ya wakazi hao na kusema kuwa ni kweli ni kilio cha muda mrefu na ili kufanikisha ujenzi wa mtaro huo zinahitajika zaidi ya shilingi milioni mia mbili ambazo tayari wameziomba serikali kuu kwa ajili ya ujenzi huo.

source.triple a fm habari/27.02.2018

No comments

Powered by Blogger.