MASHIRIKA 40 YAUNGANA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA KWENYE MASOKO JIJINI DAR ES SALAAM
Na Dotto Mwaibale
Mashirika 40 yasiyo ya
kiserikali yameungana na Shirika la Equality for Growth (EfG) katika
kukabiliana na ukatiti wa kijinsia masokoni dhidi ya wanawake.
Akizungumza mwishoni
mwa wiki kwenye mkutano wa wadau kutoka katika mashirika hayo, Mratibu wa Mradi
wa Mpe Riziki si Matusi wa EfG, Susan Sita alisema shirika hilo liliona ni
vizuri kupanua wigo wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia masokoni kwa
kuyashirikisha mashirika mengine.
"Tuliona ni
vizuri kuyashirikisha mashirika mengine katika mapambano haya ambapo mashirika
40 kutoka Manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni yalikubali kati ya hayo manne
yameanza kufanya kazi hiyo rasmi kwenye masoko ya Magomeni na Tandale wilayani
Kinondoni," alisema Sita.
Aliongeza kuwa,
mkutano huo malengo yake ni kuelezea mradi wa mfano kwa wadau na mashirika
mbalimbali yanayojihusisha na masuaya la utoaji haki ili kupanua wigo wa utoaji
wa taarifa juu ya vitendo vya ukatili vinavyofanyika kwenye masoko.
Alitaja malengo
mengine ni kuona mashirika mengine yanavyoweza kutumia mradi wa mfano wa sokoni
na kuusambaza katika masoko mengine Tanzania ikiwa ni pamoja na kuandaa
mikakati ya pamoja na namna ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia
kwenye masoko.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika hilo, Jane Magigita alisema ushirikishaji wa mashirika hayo ulianza
mwaka 2015 na kazi kubwa ya mashirika hayo ni kuwakomboa wanawake masokoni kwa
kupinga ukatili wa kijinsia.
Alitaja kazi nyingine
ni kuboresha uhusiano kati ya wanawake wafanyabiashara na maofisa wa masoko
katika kujenga uwajibikaji pamoja na kuona wanawake wafanyabiashara wa Manispaa
ya Ilala, Temeke na Kinondoni wanafanya shughuli zao kwenye mazingira huru
dhidi ya ukatili wa kingono, kiuchumi, kimwili, matusi na kisiasa huku wakipewa
heshima kama binadamu wengine na kujipatia kipato chao bila ya vikwazo.
"Tunahitaji kuona
tunafanikisha ushirikiano kati ya watekeleza sheria, kamati za masoko, viongozi
na maofisa wa Manispaa, Polisi na wafanyabiashara wote katika kudhibiti ukatili
wa wanawake katika masoko," alisema Magigita.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Pugu Poverty Alleviation and Development Agency (PPADA), Abraham
Silumbu alisema ushirikiano huo umewapa mori wa kazi kwani utasaidia kupunguza
vitendo hivyo vya kikatili masokoni nchini.
"Kwa kweli
tumeanza kuona matunda ya ushirikiano huu tumepanga mapambano haya kuyapeleka
katika masoko yote hapa nchini," alisema Silumbu.
Post a Comment