MIRADI MIKUBWA MIWILI KUMALIZA MATATIZO YA MAJI JIJINI MWANZA-WAZIRI MKUU MAJALIWA
CHANGAMOTO
ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Jiji la Mwanza kuwa
historia baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa ujenzi wa miradi mikubwa
miwili ya maji yenye thamani ya sh. bilioni 112.
Hayo
yamesemwa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Jumanne, Februari 20, 2018)
wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Halmashauri za Jiji la Mwanza,
Ilemela na Nyamagana akiwa katika siku ya sita ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri
Mkuu amesema miradi hiyo inahusisha kuboresha upatikanaji wa maji katika maeneo
ya pembezoni wenye thamani ya sh. bilioni 75 ambao utahusisha ujenzi wa chanzo
kipya cha maji kwenye eneo la Butimba chenye uwezo wa kutoa lita milioni 40 kwa
siku.
Ametaja
maeneo yatakayonufaika na mradi huo kuwa ni Butimba, Nyegezi, Mkolani,
Buhongwa, Sawa, Lwanhima, Kishiri, Nyahingi, Luchelele, Malimbe, Bulale,
Fumagila, Usagara, Kisesa, Buswelu, Nyamwilolelwa, Kahama, Nyamadoke,
Nyamhongolo, Mondo, Kiseke, Kangae, Meko, Nsumba na Bulola.
Waziri
Mkuu amesema mradi mwingine ni wa kuboresha upatikanaji wa maji katika maeneo
ya milimani wenye thamani ya sh. bilioni 37 ambao ulianza kutekelezwa Februari,
2017 na unatarajiwa kukamilika Agosti 2018.
Amesema
wakazi 105,649 wanaoishi katika maeneo ya milimani hususan yaliyo juu ya matenki
ya maji ambayo hayapati huduma kwa sasa watanufaika. Maeneo hayo ni Nyasaka,
Bugarika, Nyegezi, Capripoint, Mjimwema, Nyakabungo na Kitangiri.
Amesema
Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo,
itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na
salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi na
watendaji wa Jiji la Mwanza kuhakikisha wanashirikiana katika kuwatumikia wananchi
bila ya ubaguzi wa dini, kabila wala kipato. Pia amewataka watambue miiko na
ukomo wa madaraka yao.
Amesema
watumishi hao wanatakiwa wawe waaminifu na wasimamie vizuri matumizi ya fedha
za uetekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye maeneo yao na wahakikishe
zinatumika katika miradi husika kama ilivyoelekezwa na Serikali.
source.pmo-tripleafm-20.02.2018

Post a Comment