Mkurugenzi wa fedha NHC amrithi Mchechu Aliyetumbuliwa na Waziri Lukuvi
Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Felix
Maagi ameteuliwa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Nehemia Mchechu
aliyesimamishwa kupisha uchunguzi.
Mchechu alisimamishwa kazi Desemba 16,2017 na Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi
yake ambazo hazijawekwa wazi wala mamlaka inayochunguza.
Akizungumza jana Jumanne Desemba 19,2017 kuhusu mikakati
yake baada ya kuteuliwa na Bodi ya NHC kukaimu nafasi hiyo Maagi alisema, ‘’Kwa
sasa siwezi kusema kitu kwa kuwa hata ofisi bado sijakabidhiwa.”
“Nikikabidhiwa na nikiingia ofisini nitakuwa na cha kuzungumza
lakini kwa sasa sina cha kusema,” alisema.
Maagi ni mhitimu wa Shahada ya Uzamili katika usimamizi wa
biashara (MBA) ya Chuo Kikuu cha Esami nchini Uganda na ni mhasibu
anayetambulika na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).

Post a Comment